peperonity.net
Welcome, guest. You are not logged in.
Log in or join for free!
 
Stay logged in
Forgot login details?

Login
Stay logged in

For free!
Get started!

Mobile Blog


kidogo2009.peperonity.net

MAKALA

02.10.2010 04:28 EDT
YA SERGIE TOROP NA UJIO WA YESU WA KWELI

Na Juma Kidogo
Ni wakati mwingine tena, siku nyingine ambayo tunamshukuru Mungu kwa kuendelea kutuweka hai katika hali ya amani bila matata yoyote, wakati huu ambapo tunahesabu siku kuelekea uchaguzi mkuu. Ni wakati ambao wanasiasa huumiza vichwa kwa kujaibu kuongea na wapiga kura wao na kuwaahidi hili na lile. Nasi Watanzania tunawaomba sana watu hawa yale watakayokuwa wakiyaahidi yawe ya kweli. Mgombea wa kweli huahidi mambo machache ambayo huwa na uhakika kuwa uwezo wa kuyatekeleza atakuwa nao.

Kuliko kuahidi mambo mengi huku ukijua fika uwezo wa kuyatekeleza katika kipindi cha miaka mitano ya uongozi hauta kuwa nao. Hayo nimedokeza kidogo tu kuwakumbusha lakini si lengo la makala yangu haya ya leo. Kipindi hiki cha uchaguzi watu wanaandika sana habari na mambo yanayohusiana na uchaguzi, lakini si vibaya katika wakati huuhuu nikaachana kidogo na habari za uchaguzi na kuchepuka pembeni kidogo kwa kujadili jambo tofauti. Leo nitajaribu kujadili swala la imani, hasa nitazungumzia imani za kidini na misimamo ya waumini wake.

Yapo maswali mengi yanyojitokeza kuhusu dini hizi ambayo ni maswali yasiyokuwa na majibu. Kwa nchi za Kiafrika, hasa katika eneo hili la Afrika ya Mashariki tulipo sisi, dini ambazo ndizo zimeenea sana na kushika nafasi ni dini kuu mbili, yaani dini ya kiislamu na dini ya ukristo, japo nazo zimegawanyika katika madhehebu mbalimbali.

Katika dini hizi, wapo wanaoamini katika imani kali kabisa mpaka wanapokuwa kwenye majumba yao ya ibada hufikia hatua huangua vilio ili kuridhisha imani zao kali. Imani hiyo haikuwepo zamani, imeanza kujitokeza miaka ya hivi karibuni baada ya madhehebu kuongezeka na kuwa mengi katika hali ya kutisha. Lakini pamoja na imani hizo kali miongoni mwa wanadini na wanaimani wa sasa, yapasa turudi karne kadhaa zilizopita huko nyuma na kujikumbusha ujio wa dini zetu hizi tunazoziamini na kuzitumikia kwa nguvu zetu zote.

Wakati wamishonari na wakoloni walipokuwa wakituletea dini hizi enzi hizo, zilikuwa ni kama utamaduni wa kigeni kwa mababu zetu. Tujiulize swali moja dogo, iwapo wazee hao wa zamani wangeonyesha msimamo thabiti katika kuupinga na kuukataa utamaduni huo wa kigeni leo hii imani zetu zingekuwaje? Dini hizi mbili tangu zilipoingia zaidi ya miaka 150 sasa iliyopita zilikuta binadamu tayari wapo. Na walikuwa wakiendelea na maisha yao kama kawaida bila kutumikia vitabu wala Mungu aliyeletwa na dini hizo za kigeni.

Hapo akabla hawa walikuwa hawamtambui wala kufahamu uwepo wa Mungu mpya walioletewa. Lakini vitabu hivyo vikawaambia kuwa Mungu huyo ndiye aliowaumba wao. Hata hivyo hawakuwa na maswali, hawakukumbuka kuwauliza maswali ya msingi kwa wakati huo wageni hao waliowaletea dini mpya. Wangeuliza kuwa, wao wamekuwepo katika Afrika vizazi kwa vizazi, miongo kwa miongo na karne kwa karne. Je, ikawaje huyo Mungu aliyewaumba asiwape ufahamu wa kumfahamu tangu alipowaumba. Je Mungu aliwatelekeza babu zetu hao mpaka waarabu na wazungu walipokuja kuwafumbua macho? Pamoja na imani tuliyonayo kwa utamaduni na dini hizi za kigeni ni lazima tuwe na chembe ya mashaka japo kidogo mioyoni mwetu. Lazima tuwe na mashaka kuhusu uhalali wa dini hizi. Binadamu wote ni sawa tukiwa tumeumbwa katika miili inayofanana.

Masikio mawili mawili, mikono miwili miwili, miguu miwili miwili, macho mawili mawili, wote tumeumbwa pua zetu tundu zake zikiwa zimetazama chini. Hakuna hata binadamu mmoja ambaye tundu za pua zake zimeangalia juu na mengine mengi. Lakini dini zinakuja kuleta tofauti ki imani baina ya mtu na mtu, Wakristo wanaamini yupo Mungu, Waislamu nao wanaamini yupo Mungu. Hawa wanazungumzia Mungu huyo huyo mmoja, sifa za Mungu wa wakristo na zile za Mungu wa waislamu zinafanana sana. Lakini kinachokuja kuleta mtafaruku wa kiimani hapa ni binadamu, binadamu wanaodaiwa kuwa wao ndio waliotumwa na Mungu ili kumuwakilisha na kuwa mbadala wake wa kuhubiri amani na kufundisha njia na mbinu za kumuabudu yeye. Na sharti kubwa lililowekwa na binadamu hao ni kwamba, huwezi kumjua Mungu bila kupitia wao, wao ndiyo mawakala wakubwa wanaomuwakilisha Mungu.

Hawa ndiyo wanaoleta matatizo mpaka leo. Iwapo wamishonari wa kizungu wangekuja na kauli mbiu moja tu ya kuhimiza waafrika tumuabudu Mungu mmoja tu,na waarabu nao wangekuja na kauli mbiu ya Mungu mmoja tu bila kupitia uwakilishi wa mtu mwingine wa kati. Leo hii tungekuwa wamoja, wala makelele na vilio tunavyovisikia kwenye majumba ya ibada leo hii pengine yasingekuwepo na Waafrika wote tungekuwa na dini moja ambayo si ukristo wala si uislamu.
Pamoja na maelezo yote hayo ambayo nimeyatoa hapo juu, lengo langu kubwa lilikuwa ni kujadili ahadi ya kurudi kwa Yesu Kristo ambayo aliitoa bila ya kusema atarudi lini na katika wakati gani, hakusema pia atakaporudi atafikia katika nchi gani na atarudi kwa sura mpya, au ile ile aliyoondoka nayo.


Hakusema pia atakuja nyakati za mchana au usiku. Lakini waumini wale wenye imani kali na imani ya wastani wanapaswa kuamini maandiko hayo kuwa ipo siku nabii huyo atarudi tena duniani kwa mujibu wa biblia takatifu.
Katika mathayo 24, Yesu anasema atarudi na mualiko wa parapanda pamoja na malaika na kila jicho litamuona na atawatuma malaika zake kuwakusanya wateule wake toka mwisho huu wa nchi hata mwisho huu. Na pia anasema mataifa wataomboleza mbele zake wale waliomchoma na mwisho ndio utakuja. Pia ktk mathayo hiyo hiyo akaelezea jinsi atakavyokuja kama mwivi( kwa siri)na kutakuwa na kutwaliwa kwa mmoja na mmoja kuachwa. Mtume Paulo ktk 1wathesalonike 5 akaelezea jinsi tutakavyonyakuliwa na kwenda kumlaki Bwana mawingu na itakuwa ni kufumba na kufumbua.

Lakini hapa kuna jambo moja linanipa tabu kidogo. Jambo hilo ni kukubalika kwa Yesu Kristo atakaporudi tena duniani, ni ishara zipi zitakazowatambulisha waumini kote duniani kuwa Yesu aliyekuja sasa ndiye yeye halisi aliyeahidi kwamba atarudi na si Yesu wa bandia. Hapo juu tunaona vifungu viliyoandikwa katika biblia na mtu huyo huyo mmoja Mathayo vikipingana.

Hapa ninamashaka makubwa kuwa upo uwezekano wa Yesu mwenyewe halisi pindi atakapokuja tena duniani atakataliwa na viongozi wa kidini wa kada mbali mbali wakiwemo Wachungaji, Mapadri na hata Maaskofu wa Makanisa mbali mbali. Huu ni mtego, ni mtego ambao unaweza kuwakutanisha watu na viongozi hao wa dini katika chumba kimoja na kundi lile la Wayahudi lililomkataa Yesu na hatimae likaishia kumsulubisha hadi kumuua kikatili zadi ya miaka 2000 iliyopita. Leo hii wapo watu mfano wa Sergie Torop wanaojinadi na kutangaza kuwa wao ndiyo Yesu aliyerudi tena kuja kuukomboa ulimwengu. Wamekuja kuwarudisha kondoo waliopotea na kuwarudisha kundini.
Sergie Torop ni raia wa Siberia ya Urusi aliyezaliwa huko miaka zaidi ya arobaini iliyopita. Huyu kabla ya kuanza kujitangaza kua yeye ndiye Masiha, alikuwa akifanya kazi ya uaskari wa usalama barabarani. Hii inaamaana Yesu huyo alikuwa “trafic police” kabla ya kuanza kuhubiri na kujitangaza kuwa yeye ndiye. Tangu kuibuka kwake na madai yake hayo ya aina yake. Viongozi wa dini ya kikristo wa madhehebu mbali mbali wametokea kumpinga vikali kwa madai ya kwamba mtu huyo siyo mkweli na anaipotosha jamii ya kikristo kwa madai yake hayo.

Lakini wakati viongozi hawa wa kikristo wakimpinga na kumkataa mtu huyo, mbele ya maelezo yao wanapaswa kutuambia huyo Yesu halisi

anayesubiriwa atakuwaje, ama atakuwa na alama gani zitakazosababisha tumtambue pasi na kumtilia shaka. Na Sergie Torop ana alama gani zinazofanya akataliwe mapema na haraka kuwa yeye siye aliyekusudiwa. Ili kujiridhisha na kujiweka katika mazingira ya kutokuwa na hofu pindi atokeapo mtu wa aina ya Torop, inatubidi tutafute namna yoyote ya kuthibitisha ukweli ili kujiridhisha badala ya kumkataa mtu bila ya kuwa na ushahidi. Ipo haja ya kutumia hata vipimo vya DNA ikiwezekana ili ukweli udhihiri.

Sergie Torop,mtu anayedai kuwa ndiye yesu halisi aliyerudi upya.picha ya juu ni yesu halisi aliyeahidi ipo siku atarudi tenaVinasaba vya Yesu halilsi havikosekani, siamini kama kumbukumbu ya hata mahali ambapo mwili wa Yesu ulilazwa haukuacha chembe chembe na mabaki ya jasho lake ambayo leo yanaweza kutumika kubaini ukweli kati ya Yesu yule wa kale na huyu wa sasa yaani Sergie Torop na wengine wote wa aina yake watakaojitokeza baadae. Siamini kama ule mkuki uliotumika kumtoboa katika ubavu wake haukutunzwa mpaka leo ambapo chembe chembe zake za damu zinaweza kutumika katika kutambua ukweli.
Ikiwa Farao aliyekufa kabla ya kuzaliwa kwa Yesu Kristo mwili wake umetunzwa mpaka leo hii, siamini kama hakuna mabaki ya namna yoyote ile ya Yesu yaliyohifadhiwa yanayoweza kutumika sasa kwa ajili ya kubaini ukweli kwa sababu ki msingi Yesu alikuwa maarufu zaidi na mwenye umuhimu mkubwa katika historia kuliko Farao, vinginevyo viongozi hawa wa dini wakubali ukweli kuwa ipo siku watakuja kumkana na kumkataa kata kata Yesu halisi atakapokuja.

Lazima wakubali ukweli kwamba wao wenyewe hawajui Yesu halisi atarudi katika mtindo gani, mahali gani na wakati gani. Lazima wawe na tahadhari kuanzia sasa kabla Mungu hajawashangaa, hajawashangaa kwa kumkataa nabii ambaye huwa wakihubiri maneno na mafundisho yake kila siku hadi kufikia hatua waumini wengine kuangua vilio.

Kadri mika inavyozidi kusonga mbele ndivyo ambavyo Makanisa yanapoteza haki na fursa ya kumpokea Yesu atakaporudi tena. Karne zilizopita, Makanisa yalikuwa machache sasa lakini kutokana wa uchu wa kimaslahi wa baadhi ya wachungaji kuanzisha utitiri wa Makanisa. Je swali linakuja hapa, wakati Yesu atakaporudi mwenyeji wake atakuwa ni kanisa gani? Wanapaswa kujiuliza na kutuambua hilo mapema,vinginevyo tuambiwe tangu sasa tujue ni kanisa gani halali litakalompokea na kumakaribisha Yesu atakaporudi tena.

jumakidogo@yahoo.com 0764 561078, 0712120720


This page:
Help/FAQ | Terms | Imprint
Home People Pictures Videos Sites Blogs Chat
Top
.